KATIKA
tukio lililowaacha watu midomo wazi wasiamini kilichokuwa kikitokea,
waumini wa Kanisa la Moravian Usharika wa Boko nje kidogo ya Jiji la
Dar, walishuhudia timbwili la aina yake, baada ya waumini kugawanyika
pande mbili na kuanza kuvurumishiana makonde wakigombea madaraka.
Kwa
mujibu wa chanzo chetu ndani ya Kanisa hilo lililopo eneo la Maliasili,
mgawanyo wa makundi hayo umesababishwa na watu wawili, mchungaji wa
siku zote aliyefahamika kwa jina moja la Samweli na mwanamke mmoja
ambaye hakufahamika jina lake mara moja.
“Huyu mchungaji wa siku zote ni mtu mstaarabu sana, hana maneno na mtu,
lakini huyu mwanamama ni mtata kwelikweli,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo
chetu hicho kilizidi kutiririka kuwa, sakata la kugombea madaraka
katika kanisa hilo lenye jengo dogo na waumini wachache, limeanza kiasi
cha wiki nne zilizopita, hadi kufikia mzozo huo kusababisha mgawanyo wa
makundi mawili, kila moja likiwa na muda wake wa kufanya ibada.
Kuonyesha kuwa shetani amekuwa na nguvu kubwa katika jumuia hiyo ya
kiroho, makundi ya wafuasi hao wamekuwa wakifanyiana visa, kiasi kwamba
kundi mojawapo linapowahi na kufanya ibada, hufunga mlango kwa kufuli
aina ya solex ili kuwazuia wenzao kufanya maombi na hivyo kuzidisha
uhasama kati yao.
Kwa
mujibu wa mnyetishaji wetu, mchungaji anayejulikana na kukubalika na
wengi ni Samweli, ambaye kwa muda wote ndiye amekuwa akisalisha kanisani
hapo, tofauti na mama huyo anayedaiwa kuwa ni mkorofi.
Hata hivyo, katika hali isiyotarajiwa, baadhi ya waumini waliotengana
waliamua kumaliza tofauti zao na hivyo kuanza kusali pamoja, hali ambayo
badala ya kuleta amani sehemu hiyo takatifu, ilizidisha tafrani na
kusababisha kuzuka kwa ugomvi uliosababisha baadhi ya viongozi wa kanisa
hilo kuchaniwa mashati.
Inadaiwa
kuwa, kundi linaloongozwa na mwanamke huyo ndilo tata kuliko lile la
mchungaji, kwani upo ushahidi wa wazi kuwa amekuwa akiwaleta watu ambao
siyo waumini ili walete fujo kanisani.
Baada ya mvutano wa muda mrefu wa kupigana, kutukanana, kuchafuana na
kuchaniana nguo, hatimaye Polisi wa Kituo cha Wazo Hill, walifika eneo
la tukio na kumaliza ‘soo’ hilo kwa kuwakamata na kuondoka na watuhumiwa
pamoja na baadhi ya waumini.
Hata hivyo, Mchungaji Samweli ambaye naye alikamatwa, aliachiwa baada ya kumaliza kutoa maelezo yake.
No comments:
Post a Comment