Saturday, April 11, 2015

 

POLISI WAWADHIBITI WANAFUNZI WA VYUO VIKUU IRINGA WALIOJIPANGA KWENDA KWA LOWASSA


MAFURIKO yaliyoelezwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa kwamba hayawezi kuzuiliwa kwa mikono yake, yalitaka kutokea leo mjini Iringa kabla hayajadhibitiwa na jeshi la Polisi.
Baada ya Polisi kusikia kuwepo kwa mpango wa wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya mjini Iringa ambao ni wafuasi, wanachama na wapenzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutaka kukutana katika uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa, walijipanga na kuhakikisha hakuna wanaokutana katika uwanja huo ambao kesho utatumiwa na viongozi wa ACT, akiwemo Zitto Kabwe kuelezea sera za chama hicho.
Baadhi ya watu ukiwemo mtandao huu ulishangaa kuona magari ya Polisi yakiwa na Polisi waliojiandaa vyema na silaha zao yakiwa katika uwanja huo na mengine yakizungukazunguka barabara mbalimbali zinazoelekea katika uwanja huo.
“Leo kuna wanafunzi wa vyuo vikuu vya Iringa ambao ni wafuasi wa CCM walitaka kukutana katika uwanja huu na kutoa tamko lao linalolenga kumuomba Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa agombee urais,” alisema mmoja wa vijana waliokutwa pembeni mwa uwanja huo.
“Ni imani yetu, CCM bila Lowassa haiwezi kufanya vyema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unaodhihirisha pia jinsi wapinzani kupitia umoja wao wa Ukawa walivyojipanga,” alisema.
Kijana huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema wanataka kupeleka ujumbe kwa viongozi wa CCM wanaotaka kuendeleza hulka ya kuwachagulia watanzania viongozi wanaowataka wao.

Kutokana na ulinzi huo kuimarishwa hakuna wanafunzi waliojaribu kusogea katika uwanja huo hadi mtandao huu ulipokuwa unaenda mitamboni……..
TEMBELEA BLOG YETU KWA HABARI ZA UHAKIKA;

No comments:

Post a Comment